Mwana wa Yungi Hulewa
Mohammed Said Abdulla
Bwana Msa alikuwa kakaa juu ya kiti chake cha kulala alichokiweka pale sitahani, lakini sasa aliondoka akaenda kusimama kwenye papi za chuma nchani mwa sitaha zilizokuwa kama kizuizi au ukingo wa salama kwa abiria. Alikuwa daima kila akisafiri huweka kiti chake cha kulala hapo sitahani kwa kutaka kuona mandhari ya pwani. Chombo chao hivi sasa kilikuwa kikitambaa na bahari na kikikata maji sawasawa juu ya mawimbi ya kuumuka: hata abiria wengi, kwa hivi sasa, walikuwa wakienda huku na huku katika matembezi yao ya papo kwa papo yaliyojifinya kwa kiasi ya eneo la chombo kile kidogo. Hata nahodha aliyekuwa akiranda wa wasiwasi mkubwa hapo kwanza, chombo chake kilipokuwa kikisukasuka saa moja iliyopita na kikitishia kwenda mrama, alikuja mpaka ubavuni kwa Bwana Msa akashusha pumzi.
"W-houf! Sasa basi tumo katika salama, Bwana Msa," alisema huku akiweka mikono yake juu ya ukingo wa sitaha. Alikuwa kijana wa kiasi cha miaka ishirini na mitano tu; hata kazi ya unahodha ilikuwa bado ngeni kwake kwa vile hajawa na mazoezi ya kutosha baharini. "Unaona, Bwana Msa, ilivyokuwa," aliendelea. "Roho yangu ilikuwa juu juu wakati ule; kwani ukiona chombo kimo katika mawimbi ya kuelea, basi wewe taraji kuwa dhoruba haiko mbali, ingawa chombo chetu chenye mizani ya hali ya hewa, kilionyesha kuwa hapatakuwapo dhoruba yo yote. Lakini, kwa muda wa saa nzima ile, Bwana Msa, baada ya kuiacha tu bandari ya Dar es Salaam, roho yangu haikuwa hadhiri tena; lakini sasa nashukuru Mungu, basi tena, na Inshalla tutafika Unguja salama usalimini."
Mmoja katika abiria waliokuwa wakipita, aliacha safari yake, akawa anasikiliza maneno ya nahodha, na dalili alichapukiwa na maneno yale kwani hakutoshekwa na kusimama waliposimama wao, akajibwaga juu yake, akakaa kusikiliza kwa makini zaidi. Lakini, kama alikuwa na tamaa ya kujifunza elimu ya bahari katika maelezo machache ya nohodha, basi tamaa yake ilihukumiwa kutamauka; kwani nahodha, baada ya kutoa pumzi zake mbele ya Bwana Msa ambaye alikuwa akijuana naye tangu zamani, hakuendelea zaidi, na papo hapo aliondoka, na kwa mwendo mchangamfu, akapotea baina ya abiria kadha wa kadha waliokuwapo sitahani.
La, bwana yule hakufuata maneno ya nahodha hata yakamwekea pale; bila shaka alikuwa na lake jingine liliomvutia pale. Yameelekea kuwa ni hivyo kwa vile yeye hakufuata uamuzi wa nahodha uliomwondosha pale akaenda zake, yeye aliendelea kukaa na kumtazama Bwana Msa akitupa mafunda ya moshi hewani uliotoka katika kiko chake kisichomtoka, moshi ambao akiutema tu hewani, mara papo hapo hupanguswa na upepo, usionekane ulikoishia.
Bwana yule alikuwa rika moja na nahodha, bali yeye alikuwa mtu wa rangirangi. Uso wake ulikuwa mzuri, kwa uzuri uliokwenda na wanaume. Na, kwa rangi yake na sura yake, ilikuwa shida kuweza kumweka sawa katika kabila ya ukoo wake—kama ni Mwarabu au ni Muhindi, bali alikuwa kati na kati, au kokote utakakomwelekeza utamwona yuko. Kitu kilichoonekana wazi usoni mwake, kikawa kama ni alama yake, kilikuwa ni shama au chunjua iliyokaa pembeni karibu na mdomo wake wa chini. Nguo alizovaa zilionyesha hali yake ya ulitima aliyonayo—suruali ya kaki kuukuu na shati la kaki kuukuu liliochanika mwisho wa lisani yake likaacha tumbo lake kidogo li wazi; na mabegani, huku na huku, limeshonwa likashonwa tena hata likamfanya kama kavaa tepe.
Bwana Msa alipoona ana mgeni, aliona vile vile kuwa ana mtu wa kuongea naye. "Binadamu anajasurisha vibaya," alianza. "Ee, kuaminisha kujitia katika kifuu kama hichi, akakiacha kicheleze katika bahari kuu kama hii, sijui pima ngapi kwa kwenda chini, hana kitu cha kushika hata kimoja—si anapeleka posa za kujitakia uchumba na mauti? Watu wa zamani hawakukosa walipokiita chomba cha baharini 'Mungunitwae!'
"Bwana wewe," alijibu yule kijana, akitafuta la kusema, "nimemsikia nahodha pale akikwita 'Bwana Msa.' Tuseme wewe ndiye yule 'Bwana Msa' maarufu, mbayani anayevuma kwa uhodari wake wa upelelezi wa siri . . . na kwa uhodari wake huo hata watu wengine wamefika hadi ya kumfikiri kuwa si mtu bali ni jini, mbali wale wanaomwita Sherlock Holmes wa Unguja . . . ?"
Bwana Msa alikunja uso, kwani aliona kazi hiyo imemfikia wakati ule; alipepesa akapesapesa, kisha akasema, "Sijui nikujibu nini, bwana mdogo."
"A-aa, miye nakuuliza tu, bwana," alijibu yule kijana. "Nimesikia ukiitwa 'Bwana Msa,' nikaona enhe, leo nitamjua Bwana Msa; ndipo nilipokuuliza kama wewe ndiye—"
"Ndiye nani?" alidakuliza Bwana Msa kwa kumaka. "Umeniuliza kama mimi ndiye—ndiye mpelelezi wa siri, siyo? Au jini? Au Sherlock Holmes wa Unguja? Kama hayo ndiyo unayotaka kuyajua, basi mimi si mpelelezi wa siri, wala si jini; wala si Sherlock Homes." Bwana Msa alionyesha kahamaki; au, akali, hakupendekezewa na mambo aliyoleta kijana yule. "Lakini wewe ndiye Bwana Msa?" "Ndiye." "Achilia mbali jini au Sherlock Holmes—lakini, pia, wewe si mpelelezi wa siri?"
"Si mpelelezi wa siri, mimi ni mchunguzi wa mambo."
"Ah," alighumiwa yule kijana, "kwani kuna tofauti baina ya mpelelezi wa siri na mchunguzi wa mambo?"
"Naam, tena kubwa."
Kijana yule hakutaka kuijua tofauti iliyopo, bali alimhujumu Bwana Msa kwa upande mwingine. "Lakini unajua, bwana," alianza tena, "kuwa, kuna mtu aliyekusanya visa vyako katika vitabu mbali mbali, maarufu katika hivyo amekiita Mzimu wa Watu wa Kale, na humo kakutoa wewe kama ni mpelelezi wa siri hodari sana?"
"Unadhani tu," alijibu Bwana Msa kwa kumaka, "na wengine kama wewe, pia, wanadhani tu; lakini, akutukanaye ni maalum hakuchagulii tusi, na tusi lililo mbelembele kwenu la kunisambikiza nalo ni hilo la kuniambia mimi ni mpelelezi wa siri."
"Kwani mtu kuwa mpelelezi wa siri ni tusi, bwana?"
"Naam, tusi kubwa sana,hasa kwangu mimi, na kadhalika kwa mtu ye yote mwenye heshima yake. Kama mpelelezi wa siri si tusi, acha tukwite wewe, basi kama utakubali. Kwa Sherlock Holmes, kweli. Kwa Sherlock Holmes, upelelezi wa siri ulikuwa ni sifa ya utukufu wake."
"Ajabu hii," alijibu yule kijana, akiinamisha uso wake kutazama chini. "Nasema ajabu hii," alinyanya uso wake kumtazama Bwana Msa, "mtu kusifiwa kwa uhodari wake alionao katika upelelezaji wa siri, na yeye aone katukanwa!"
Alinyamaza kidogo, kisha akaibuka kwa ghafla na swali mkataa. "Bwana wewe, unakubali kuwa yale yaliyoandikwa katika kitabu kile Mzimu wa Watu wa Kale ni kweli?"
"Nakubali," alijibu Bwana Msa bila kimeme wala kusitatasita.
"Kama wewe ndiye Bwana Msa, basi mimi nimekisoma kitabu kile na nimeona uhodari wako mkubwa wa upelelezi wa siri uliyotunonyesha katika kadhia ile—hata yule spekta wa polisi, nani vile, Spetka Seif, kashindwa na wewe katika kazi hiyo. Unasemaje, bwana?"
"Nasema," alijibu Bwana Msa pole pole, "kuwa mimi nimekisoma kitabu hicho; tena mimi nimekisoma mbele kuliko mtu ye yote mwingine, maana yeye mweneyewe, huyo aliyekiandika, aliniletea mimi nikisome tangu kimo katika mswada tu, ili niangalie alivyoandika. Na mimi, bwana wewe, sikuona hata mahali pamoja—licha kuandika wa uwazi na kwa kinaganaga—kama unavyonielezea wewe, bali hata kwa kudokeza tu—aliposema kuwa mimi ni mpelelezi wa siri. Na kama angalinipaka ma -i - uchafu huo katika uzembe wa porojo lake, basi mimi ningalimshtaki nikampleke mbele ya mahakama kuu kwa hatia ya kunivunjia heshima yangu; umetoshekwa sasa?
"Oo-oh! Bwana wewe ni mtu wa ajabu kweli kweli," alishangaa yule kijana, "hivyo kweli kweli unakana kuwa wewe umefanya upelelezi wa siri katika kadhia ile?"
"Ndio, nakana."
Kimya, Lakini mara kijana yule alizuka na maonyo ya kweli. "Bwana Msa—maana sasa nimekwisha kulijua jina lako hasa—tafadhali nisamehe kwa haya ninayokwambia. Sikusuti, hasha, lakini napenda kukukumbusha tu. Siye wewe uliyemtambua nani aliyemwua Bwana Ali? Siye wewe uliyetambua kuwa Bwana Ali kauza mali yake yote kwa yule Banyani, Seti Sumatra? Siye wewe uliyetambua kuwa Bwana Ali hakuuliwa mzimuni, ila kiwiliwili chake tu ndicho kilichopelekwa mzimuni, ukawajua na watu wenyewe waliokipeleka huko na mengi mengine ya siri yaliyokuwa yamejificha, na hakuna mtu aliyeyafichua ila wewe?"
"Naam, mimi," alijibu Bwana Msa, huku akimtazama yule kijana usoni kama kumwambia 'Ndio nini?'
"Umeyajua yote yale na wewe hukufanya upelelezi wa siri?"
"Sikufanya upelelezi wa siri."
"Basi, Bwana."
"Si basi kamwe—bado," alijibu Bwana Msa kwa sauti ya mkazo juu ya 'kamwe' na 'bado'; dutu la uso wake likionyesha uzingativu na azimio la ukaidi. "Unasema mimi naambiwa kuwa ni Sherlock Holmes wa Unguja, siyo?" alianza Bwana Msa. "Hebu mtazame Sherlock Holmes alivyokuwa. Sherlock Holmes alikuwa kazi yake upelelezi wa siri, au kama unavyojulikana kwa lugha ya kwao, private detective, na watu huenda kumwajiri akawafanyie upelelezi wa siri. Mpaka hivi sasa, nani aliyeniajiri mimi kumfanyia upelelezi wa siri? Katika Mzimu wa Watu wa Kale, hicho kitabu ulichokitaja, hamna Sherlock Holmes aliyeajiriwa, hakuwamo mpelelezi wa siri, nilikuwamo mimi, Bwana Msa, mtu tu, nimefuatana na rafiki zangu wawili Najum na Ahmed kwenda kutembea shambani kwao Ahmed – basi! Sasa huyo mpelelezi wa siri katoka wapi? Ilitokezea tu mimi kuwapo kule, na nikapendezewa tu kufanya uchunguzi wangu mwenyewe, na bila shaka utakubaliana nami kuwa ipo tofauti kubwa baina ya mchunguzi wa mambo anayechunguza mambo kwa hiari yake, na yule mtu anayefanya kazi ya upelelezi wa siri kwa ujira. Tofauti ya 'kuchungua' na 'kupeleleza' ni hii kwamba 'kuchungua' ni kutazama kwa bidii pamoja na uangalifu na usikivu ili kupata ukamilifu wa jambo, hata uweze kukatia kuwa hili limekuwa hivi kwa sababu fulani tu. Na 'kupeleleza' ni kuduhushi na kudukiza jambo kwa kulidunzi pamoja na kulipekua na kulichakura."
"Kwa hivyo, bwana, nakubaliana na wewe," alikubali yule kijana, "kwa sababu hakuna aliyekuajiri kumfanyia kazi ya kuduhushi, kwenda kudukiza na kumpekulia jambo. Katika mote nilimosoma habari zako nimeona kuwa jambo hutokea na ikasadifu tu kuwa na wewe upo; tena hapo ni kupenda kwako wenyewe tu kujishughulisha kulichunguza, mfano kama riyadha kwako—ila, labda, mara moja tu, nawe bado hukuajiriwa, bali uliombwa kwa kubembelezwa na msichana yule—nani vile?—Mwanatenga, uende ukamtafutie mchumba wake, Saidi; tusisahau vile vile ulipoombwa na yule spekta wa polisi kumsaidia kutafuta mali ya yule bwana tajiri mkubwa, Bwana Hakimu Marjani. Barabara, Bwana Msa."
"Basi ni hivyo, bwana," aliakidi Bwana Msa. "Kama hivi sasa," alianza tena, "nikikwambia kuwa wewe ni mtu wa Unguja, itakuwa nimekupeleleza; nikikwambia kuwa hali ya maisha yako si nzuri—hata naweza kusema kuwa nguo hizo ulizovaa ndizo zizo hizo, huna nyingine za kubadili—itakuwa nimekupeleleza (kijana yule alijitazama huku na huku akainamisha uso chini); nikikwambia kuwa umeondoka Unguja kwenda Dar es Salaam kwa matarajio ya kutengeneza hali yako, na huko hukufanikiwa na kitu, itakuwa nimekupeleleza; nikikwambia kuwa hivi sasa unarudi Unguja kwa kuwa una matarijio mema, tena unarudi kwa nauli si yako, itakuwa nimkupeleleza; nikiwa . . . "
"Basi Bwana Msa, basi bwana!" aliruka yule kijana kakiacha kiti akasimama wima. "Taile, bwana; mbukua hiyo."
Bwana Msa alimtazama yule kijana, shingo kaweka upande, kisha alimwuliza, "Mbona unaniambia taile—mbukua; kwani nimefichua siri yako, bwana?"
"Naam, yote uliyoyasema hapa, ndiyo. Acha watu wakuite jini. Na ilivyofika hadi hii—wapi tutapata—napenda kukuzungumzia habari zangu, Bwana Msa."
"Hapa hapa," alijibu Bwana Msa. "Kwani hapa pana nini? Tumekaa tunazungumza tu, nani atatushughulikia? Wewe rudi ukae kitini kwako, na mimi nimesimama nakusikiliza—unasemaje?"
"Haya." Kijana yule alirudi kukaa kitini akanyanyua uso kumtazama Bwana Msa. Bwana Msa alikuwa akiwasha kiko chake kilichomzimikia kwa ghafla. Hapo tena kijana yule alianza hadithi yake.
"Bwana Msa, mimi jina langu naitwa Amanullah, na tangu kufunua macho yangu najiona nalelewa na bibi mmoja kule Kwahani—sijui kama yuhai bado—akiitwa Binti Abdalla. Nitakwambia kwa ufupi tu, Bwana Msa. Si peke yangu niliyekuwapo ulezini kwa bibi huyo, bali tulikuwa watoto wanne sote sote, wake kwa waume. Lakini mimi na mtoto mmoja wa kike anaitwa Sichana ndio tuliokosa bahati kwa yule bibi, sijui kwa sababu sisi tuna vichunjua mashavuni mwetu, maana kuna watu wengine wanaochukulia kuwa mtu mwenye chunjua au shama usoni kwake ni mtu mwenye kisirani au mchimvi, basi labda hivyo."
"Miaka miwili ilyopita bibi yule alitugeukia mimi na Sichana kabisa kabisa, hata chakula tulikuwa hatupewi ila cha kurambaramba tu, achilia mbali nguo na pesa za kutumia. Hayo yalikwenda kwa muda wa miezi mitatu, na mwezi wa nne bibi yule alitwambia mimi na Sichana tuhame kwake maana yeye hana tena uwezo wa kutuweka na kutukimu kwa mahitajio ya maisha yetu. Hiyo ilikuwa ni kazi, Bwana Msa, na mastaajabu yangu niliyokuwa nayo ni kwamba mbona sisi watu wawili tu, mbona wale wenzetu ambao ni watoto wa kulea vile vile, hawakufikishiwa idhilali ile wala hawakuambiwa kutafuta pa kwenda?
"Elimu yangu ya chumba cha nane haikuweza kunipatia nafasi ya kazi; kwa hivyo, ilinilazimu kutafuta kibarua cho chote, na nikapata kazi ya kuponda udongo katika Idara ya Papliki. Pesa za mwezi wa kwanza nikatafutia chumba kule kule Kwahani, tukahamia mimi na Sichana ambaye na yeye, kwa bahati nzuri, alipata kazi ya kulea mtoto wa bwana mmoja aliekuwa karani katika idara mojawapo ya serikali—kazi ya kutembea na mtoto huyo katika kigari chake wakati wa alasiri. Mimi na Sichana, Bwana Msa, tulikaa kama bibi na bwana, na tukajiburura kwa hali zetu kama hivyo kwa muda wa miezi mitatu. Baada ya miezi mitatu hiyo ilikuja kupunguzwa watu kazini kwangu, na mimi nikawa mmoja katika hao waliopunguzwa. Taabu ilizidi kwa vile mchumaji sasa alikuwa Sichana tu.
"Hapa, Bwana Msa, sijui kama utaniona nina akili au nina wazimu. Si mara mbili wala si tatu, kulinijia usingizini kuota kama mtu ananiambia, 'Nenda Darsalama; mafanikio yako yako Darsalama.' Ndoto hiyo ilipojirudishia mara kwa mara, hamu ya kwenda Darsalama ilinikaa rohoni; na mwisho nilifanya shauri na Sichana, tukaafikiana kuwa bora nitawakali kwa Mungu, asaa. Na Sichana alifanya mpango wa kukopa pesa kwa tajiri wake, nikapata nauli ya kwenda Dar. Kule nilifikia kwa sahibu yangu mmoja niliyejuana naye nilipokuwa kazini. Namshukuru bwana huyo kwa kunipokea na kujaribu kunipatia kazi. Lakini siku zilikuwa zinakwenda, na kazi ilikuwa mbali na mimi, acha kuipata hata kuipatia. Hata nafsi yangu ikawa taabani kujigandisha kwa mtu tu kwa kula na kulala—lakini nifanyeje?
"Juzi, sahibu yangu aliporudi kutoka kazini, aliniambia kwamba ameitwa polisi akaulizwa habari zangu. Kaulizwa kama kwake kapata mgeni kutoka Unguja mwenye wasfu kama wangu, na yeye akakubali kuwa anaye mgeni wa Unguja mwenye wajihi huo, kwani polisi hawakuacha kumtajia alama yangu kubwa ambayo, unaiona Bwana Msa, shavuni kwangu, hii shama iliyoko karibu na mdomo wangu, shama ambayo imekaa kama ndiyo kisirani changu, hata kama nitataka kujificha, shama itanifichua. Na alipoulizwa jina langu akawatajia kuwa naitwa Amanullah, ikawa ndio kabisa, ndiye mimi hasa mtu wamtakaye.
"Kwa namna alivyonieleza sahibu yangu, mimi ilinijia hofu. Natakiwa na polisi—nimefanya nini jamani, mimi mgeni wa Mungu, katika ardhi ya Mungu wasaa, nchi ya watu, natafuta maisha?
"'Mafanyikio yako yako Darsalama,'" alidokeza Bwana Msa huku akiwasha toza yake. "Si umekwenda kuyatafuta?"
"Mafanikio ya kutafutwa na polisi, Bwana Msa?" alijibu yule kijana. "Basi hayo si mafanikio, hayo ni maafa. Lakini sahibu yangu papo hapo aliniweka sawa, akaniambia nisishtuke, mambo yenyewe yote ni ya heri na salama. Yuko mtu huko Unguja ananitafuta, na anasema kwamba yeye ni 'mzee wangu'; kaleta barua katika mikono ya serikali na hundi la posta kwa jina langu, nikapokee posta Sh. 200/-, nifanye safari ya kurudi Unguja, na yeye huyo 'mzee wangu' nitamkuta gatini, ananingoja.
Tulifuatana mimi na rafiki yangu mpaka polisi, na huko nilonyeshwa hiyo barua waliyopokea kutoka kwa 'mzee wangu.' Mimi, Bwana Msa, hukosi umefahamu katika kielezo changu, siwajui wazee wangu. Lakini, mastaajabu si hayo, huyo 'mzee wangu' anayeniita huko Unguja, ana jina la Kigoa—Soarez, na jina langu mimi si Amanullah, bali Emmanuel. Kukataa mbele ya polisi kuwa Goa huyo si mzee wangu, ilikuwa kinyume na muhali kabisa, maadam mimi siwajui wazee wangu, na mazali yeye, huyo 'mzee wangu' kataja alama yangu kubwa na kaitia muhuri wa jina langu. Kajuaje alama yangu na jina langu kama mtu huyo hana bayana ya kweli iliyonitenga mimi na watu wengine?
"Kwa hivyo, nilipokea hundi yangu, nikaenda posta kupokea pesa zangu, nikatengeneza safari, na hivi sasa ndiyo narudi Unguja nikaonane na 'mzee wangu' wa Kigoa. Hii ndio habari, Bwana Msa."
"Nzuri," alijibu Bwana Msa, na bashasha juu ya uso wake. "Hii inathibitisha kuwa kiko kitu katika ndoto, si upuzi tu kama wengi katika sisi tunavyozikadiria. Na itakuwaje ndoto ziwe upuzi, na katika Kurani tukufu zimetajwa, tena kwa namna ya kutufafanulia kuwa kila ndoto ina maana yake? 'Nenda Darsalama; mafanikio yako yako Darsalama,'—unaambiwa usingizini—umekwenda Dar;' unaona mafanikio yako yanakuja? Dalili ya heri ni kule kuletewa Sh. 200/- kwanza za kufanyia safari ya kurudi kwenu, na aliyekuletea ni mtu hata humjui nani! Nani anajua, ila Mungu tu, jambo gani litakuwa utakapofika Unguja?"
"Inshalla heri, Bwana Msa," aliomba Amanullah.
"Amina," alibariki Bwana Msa. "Nakuombea heri na baraka za kazole, inshalla." Bwana Msa alisita kidogo kuwasha kiko chake. "Ndoto yako inanikumbusha hadithi moja," alianza tena Bwana Msa, "Hadithi niliyoisoma zamani—si hadithi, bali ni kweli hasa imetokea. Mtu mmoja wa Bara Hindi," aliendelea, "alikuwa katika ulitima mkubwa, kama wewe Amanullah. Mtu huyo aliota hivyo hivyo mara kwa mara kama mtu anamwambia, 'Riziki yako iko Misri, nenda Misri ukaichukue.' Tangu alikuwa akiona upuzi mpaka akaitia maanani, akaamua kwenda Misri. Fikiri masafa ya tangu Bara Hindi mpaka Misri! Na yeye hana nauli ya kipando cho chote kile! Alikwenda mtu huyo kwa miguu kwa muda wa miezi mitatu. Alipofika Misri, ulikuwa wakati wa magharibi, akapata msikiti akaingia kwa nia ya kulala humo mpaka asubuhi.
"Usiku wa manane," aliendelea Bwana Msa, "aliingia mwizi katika nyumba jirani na msikiti ule. Wenyewe walikuwa wamacho, wakapiga kelele za kamsa, na mwizi akakimbia. Wale waliokuwa wakimfukuza, waliona hapana ila mwizi yule kaingia mle msikitini; na walipoingia humo walimkuta yule mgeni wa bara Hindi, wakamkamata kuwa ndiye mwizi wao. Mgeni yule, masikini, alitapatapa, lakini hakuwapo mtu wa kusikiliza maneno yake; asubuhi alipandishwa mahakamani.
"Huko alipata nafasi ya kueleza habari yake tangu mwanzo hadi hatima, na kadhi aliyesikiliza kesi yake, alimsikitikia sana, kisha akamshutumu—vipi yeye kutoka Bara Hindi kuja Misri kwa miguu kwa kufuata ndoto tu?
"Mimi mara ngapi naota," alisema hakimu, "kuwa Bara Hindi katika mtaa kadha (akautaja mtaa wenyewe), katika nyumba namba kadha; katika ua wa nyumba hiyo kuna mfereji; chini ya mfereji ule kuna hazina, niende nikaichukue; na mimi hata sikushughulika. Vipi niache yangu huku, nifuate ndoto tu? Si wazimu huo?"
"Hakimu alimhukumu mtu huyo," alimaliza Bwana Msa, "afungiwe safari ya kurudishwa kwao siku ile ile kwa nauli ya serikali.
"Sasa basi, mtaa alioutaja yule hakimu kuwa kaambiwa katika ndoto yake, ndiwo mtaa alikokuwa akikaa yule mgeni wa Bara Hindi, na nyumba yenye namba aliyoitaja yule hakimu, ndiyo nyumba aliyokuwa akikaa yule mgeni wa Bara Hindi. Na yeye alipofika tu kwao na kwake, haikuwa vigumu kwake kwenda kufukua chini ya mfereji na kuitoa hazina iliyozikwa hapo! Ilikuwa lazima aende Misri kwanza ndiyo aipate riziki yake—unaona basi, Amanullah!" Bwana Msa alimaliza.